Sifa za Kujiunga JWTZ (Vigezo vya Kujiunga Jeshi), Historia ya kazi na shughuli za ulinzi na usalama hapa Tanzania zilianza tangu zama za mababu zetu. Jamii nyingi zilizoishi katika maeneo mbalimbali hapa nchini zilikuwa na ulinzi wa jadi uliohusisha kila mwanajamii. Ulinzi wa jadi ulikuwa msingi wa usalama wa jamii zote kwa wakati ule. Silaha zilizotumika na mababu zetu zilikuwa duni kama vile upinde, mikuki, mundu, mapanga na sime kama silaha za msingi kulinda jamii zao. Kila kabila lilikuwa na namna ya kuwaandaa vijana wao kujifunza matumizi ya silaha na baadaye vijana walipewa jukumu la kulinda jamii zao.
Bara la Afrika lilipata mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii baada ya Mapinduzi ya Viwanda yaliyotokea huko Ulaya katika karne ya 19. Mkutano Mkuu wa Berlin uliofanyika kuanzia mwaka 1884 hadi 1885 ulifuatiwa na mabadiliko makubwa ya nchi za Afrika kutawaliwa kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Huu ndiyo mwanzo wa nchi nyingi barani Afrika kuanza kuwa chini ya majeshi ya kigeni.
Ujerumani ilijipatia uhalali wa kuitawala Tanganyika baada ya Mkutano wa Berlin ulioligawa Bara la Afrika katika vipande vya nchi bila ridhaa ya Waafrika wenyewe. Jeshi la Kijerumani lilianzisha harakati za kufuta tawala za makabila mbalimbali hapa nchini ili kuwa na utawala mmoja na jeshi moja la kikoloni. Harakati hizo za Wajerumani zilipelekea baadhi ya makabila kupambana na Jeshi la Kijerumani, kwa vile utawala wa Kijerumani ulilenga kuharibu mfumo mzima wa ulinzi wa jadi, siasa na uchumi wa wenyeji.
Vita ya Chifu Mkwawa na Vita vya Majimaji
Vita ya Chifu Mkwawa mwaka 1890 ni mfano kamili unaoonesha kuwa baadhi ya makabila hapa nchini yalikuwa na ulinzi imara japokuwa yalikuwa yanatumia silaha duni. Hata hivyo, miaka michache baada ya Chifu Mkwawa kushindwa vita na Wajerumani, kulianza vita vya Majimaji iliyopiganwa kuanzia mwaka 1905 hadi 1907. Vita hiyo iliiweka historia ya Tanganyika katika ramani ya dunia kwa kuwa makabila mbalimbali yalitumia silaha zao za jadi kupinga uvamizi wa majeshi ya kigeni, lakini kwa umoja wao walisimama kidete kupambana Uafrika wao.
Kipindi hicho cha kuligawa Bara la Afrika kilileta mabadiliko ya kiulinzi na kiusalama kwa vile Waafrika walinyang’anywa haki yao ya kujilinda na ndiyo ukawa mwanzo wa majeshi ya kisasa kuanza kutumika hapa nchini.
Harakati za kijeshi hapa nchini ziliingia katika sura mpya baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kuanzia mwaka 1914 hadi 1918. Wajerumani walipoteza na kunyang’anywa makoloni waliyokuwa wanayatawala kama sharti mojawapo la kushindwa vita. Tanganyika iliwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza na kwa udhamini wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kuanzia kipindi hicho muundo wa Jeshi rasmi lililoongoza Tanganyika lilijulikana kama Kings African Rifles (KAR).
Sifa za Kujiunga JWTZ
Utaratibu wa Kujiunga na JWTZ
Mtu yeyote ataandikishwa kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa sifa zifuatazo:
- Awe raia wa Tanzania
- Awe na Elimu ya Kidato cha Nne na kuendelea na awe amefaulu
- Awe hajaoa/hajaolewa
- Awe na umri kuanzia miaka 18 hadi 25
- Awe na tabia na mwenendo mzuri
- Awe na akili timamu na afya nzuri
Masharti ya Utumishi
Askari atapewa nambari ya utumishi baada ya kufaulu mafunzo ya awali. Atalitumikia Jeshi kwa kipindi cha mwanzo cha miaka sita, baada ya hapo atafanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili miwili kwa kibali cha Mkuu wa Majeshi.
Maafisa
Bodi ya Uteuzi wa Maafisa (Officers Selection Board) huwafanyia usaili Askari wenye elimu ya Kidato cha Sita na kuendelea toka Vikosini na Shule za Askari wapya (Recruitment Schools). Watakaofaulu masailiano hayo hupewa hadhi ya Afisa Mwanafunzi (Officer Cadet), na hupelekwa Chuoni (Tanzania Military Academy) kwa mafunzo ya Uafisa kwa muda wa mwaka mmoja.
Taarifa Zaidi: https://www.tpdf.mil.tz/
Soma Zaidi:
Tuachie Maoni Yako